Share
By Denviz Mwazighe
Iwapo ujenzi wa Zahanati ya Baghau-katika wadi ya Ronge utakamilika kwa wakati, basi itakuwa afueni kubwa kwa wakaazi wa maeneo ya Baghau, Msangachi,Mdundonyi na Kironge, ambao hulazimika kutembea mwendo mrefu kutafuta huduma za matibabu.
Katika mahojiano na wakaazi wa maeneo hayo wakiongozwa na mwenyekiti katika ujenzi wa zahanati hiyo Bi. Mercy Mwatabu, ameeleza kuwa tangu taifa kujipatia uhuru wamekuwa wakitembea zaidi ya kilomita nane au hata kumi kutafuta matibabu katika zahanati za Iriwa, Msau na Mwambirwa.
Wakaazi hao wanaeleza kuwa umbali huo wa kupata matibabu umekuwa ukiwahatarishia maisha hasa wanawake wajawazito na watoto,ambapo pia wamesema kutokana na ubovu wa barabara uchukuzi wa magari wakati wa mvua hutatizika, hiyo kuwaweka hatarini wagonjwa na wanawake wanaofikia muda wa kujifungua.
Kauli sawia na hiyo imetolewa na mzee Justine Mwachala,mkongwe wa miaka 75,ambaye anahoji kutembea mwendo mrefu kutafuta matibabu kumekuwa ni changamoto kubwa kutakana na umbali ulipo kuzifikia zahanati hizo.
Ujenzi wa zahanati ya Baghau uliratibiwa kuanza mwaka 2020 kwa makadirio ya shilingi milioni 1.5, na ulifaa kukamilika mwezi Juni mwaka huu wa 2021,ila kufikia sasa ujenzi huo bado haujakamilika. Vile vile kaunti ya Taveta ilikadiria kutenda shilingi bilioni 1.19 kuendeleza miradi ya maendelezi kwa kipindi cha miaka tano kati ya mwaka wa 2018 hadi 2022.
Kulingana na mwanakandarasi katika ujenzi huo,ni kutokana na ubovu wa barabara ambao umekuwa ukiathiri usafirishaji wa vifaa vya ujenzi.
Aidha juhudi za kituo hiki kupata taarifa kutoka kwa wizara ya ujenzi kaunti ya Taita Taveta zimekua zikigonga mwamba, kwani waziri katika wizara hiyo amekua hapokei wala kujibu jumbe zetu.
Picha: Huduma za afya kaunti ya Taita Taveta. Source: KNA
Makala haya yameletwa kwako na Mwanedu Fm kwa ushirikiano na Code For Africa, Kenya Community Media Network na Baraza La Vyombo Vya Habari Katoliki (Cameco) kupitia msaada kutoka Ushirikiano wa Ujerumani kama sehemu ya mradi Kaunti Yetu Jukumu Letu